Mtume Petro

Simoni Petro alikuwa Myahudi wa karne ya 1, mfuasi wa Yesu Kristo, tena kati ya wandani wake.

Mtume Petro
Mtakatifu Petro katika mavazi ya Kipapa alivyochorwa na Peter Paul Rubens katika karne ya 17.
Mitume wa Yesu
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Jesus
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Baada ya Yesu, ndiye mtu anayejulikana zaidi katika Injili zote nne.

Katika orodha zote nne za mitume 12 wa Yesu zinazopatikana katika Biblia ya Kikristo anashika nafasi ya kwanza (tofauti na wenzake wengi ambao wanabadilishana nafasi, na kinyume cha Yuda Iskarioti, msaliti anayepewa daima nafasi ya mwisho); isitoshe Math 10:2 inasisitiza nafasi yake hiyo: "Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro".

Tangu kale Wakristo wengi, hasa Wakatoliki na Waorthodoksi, wanamheshimu kama mtakatifu, tena kama papa wa kwanza wa Roma hadi kifodini chake kati ya miaka 64 na 67, wakati wa dhuluma ya Dola la Roma dhidi ya Ukristo iliyoanzishwa na Kaisari Nero.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila tarehe 29 Juni pamoja na ya Mtume Paulo.

Jina lake

Mwana wa Yona au Yohana, jina lake asili kwa Kiebrania ni שמעון, Šim‘ôn, Shim'on (kutoka kitenzi shama yaani "kusikiliza").

Kadiri ya Injili ya Mathayo (16:18) na Injili ya Yohane (1:42) ni Yesu Kristo aliyembadilishia jina akamuita Kefa (kwa Kiaramu "mwamba", jina ambalo lilitafsiriwa kwa Kigiriki Petros na kwa Kilatini Petrus).

Mtume Paulo alimtaja kwa kawaida kama Kephas (1Kor 1:12; 3:22; 9:5; 15:5; Gal 1:18; 2:9,11,14) na mara moja kama Petro (Gal 2:7-8).

Maisha yake ya awali

Mzaliwa wa Bethsaida, kaskazini kwa Galilaya, alihamia Kapernaumu pamoja na ndugu yake Andrea kwa ajili ya uvuvi kwenye ziwa Galilaya. Kijiji hicho kikawa baadaye makao makuu ya utume wa Yesu katika maeneo ya kaskazini ya Palestina. Hasa Yesu alitumia nyumba na boti la Petro.

Mtu wa ndoa, Petro hakusomea ualimu wa Torati, lakini alimfuata Yohane Mbatizaji. Akiwa kwake, karibu na mto Yordani, aliletwa na Andrea kwa Yesu (Yoh 1:41-42).

Baada ya kukutana na Yesu

Aliitwa na Yesu kumfuata wakiwa huko ziwani (Math 4:18-20 ; Lk 5:11) akiahidiwa atakuwa "mvuvi wa watu", halafu akafanywa mtume wake wa kwanza.

Pamoja na Mtume Yakobo Mkubwa na Mtume Yohane, wana wa Zebedayo, alishirikishwa matukio kadhaa ya pekee kama mwandani wa Yesu, hasa aliposhuhudiwa na Mungu mlimani huku ameng'aa kiajabu (Mk 9:2-9).

Akiwa na silika ya uchangamfu, alikuwa msemaji mkuu kati ya mitume wa Yesu; hasa walipoulizwa naye wanamuona kuwa nani, akajibu: "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai" (Math 16:16). Ndipo alipojibiwa na Yesu: "Heri wewe Simoni Bar-Yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni" (Math 16:17-19).

Ungamo la namna hiyo linaripotiwa na Yoh 6:68 pia: "Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu".

Mara nyingine majibu yake yalimvutia lawama ya Yesu, hata akaitwa "Shetani" kwa sababu ya kumshawishi aende mbali na matakwa ya Mungu ili afuate mbinu za kibinadamu (Mk 8:33).

Kwa kuwa Yesu alitakiwa kutumikia, akawafundisha wafuasi wake kutumikia, Petro aliagizwa kuandaa pamoja na Yohane karamu ya mwisho ya Yesu na mitume wake kwenye Pasaka, ambapo ilimbidi akubali kuoshwa naye miguu (Yoh 13:8-9).

Yesu alipokamatwa, Petro alijaribu kumtetea kwa upanga, halafu akamfuata kwa mbali pamoja na Yohane mpaka ndani ya ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Ndipo woga ulipomfanya amkane Yesu mara tatu kwa kiapo kama alivyotabiriwa naye.

Hata hivyo, Yesu alikuwa amemuahidia atamuombea aongoke akaimarishe wenzake: "Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako" (Lk 22:31-32). Basi, alipotazamwa na Yesu akajuta kwa machozi mengi.

Baada ya ufufuko wa Yesu

Baada ya kifo cha Yesu, akawa wa kwanza kuingia kaburi lake tupu, tena wa kwanza kati ya mitume kutokewa na Yesu mfufuka Jambo hilo ni kati ya kweli zilizotakiwa kuungamwa na Wakristo wa kwanza: .

Katika tokeo lingine katika ziwa Galilaya Yesu alimthibitisha katika uongozi wa kundi lake lote, kondoo na wanakondoo. Alifanya hivyo baada ya Petro kukiri mara tatu kwamba anampenda (Yoh 21:17): "Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda".

Kadiri ya Matendo ya Mitume, kabla ya ujio wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste ya mwaka huo (30 au 33 B.K.) aliongoza wafuasi wake kuziba pengo la Yuda, mtume msaliti, kwa kumweka Mathia mahali pake .

Halafu akawa mhubiri shujaa akachukua maamuzi muhimu sana kwa uenezi wa Kanisa, kama vile kubatiza akida Korneli na Wapagani wengine bila kudai watahiriwe kwanza .

Jambo hilo lilimvutia lawama kubwa, lakini zikaja kwisha hasa kwa mtaguso wa Yerusalemu (mwaka 49).

Petro alikuwa maarufu kwa miujiza pia, kiasi cha kuponya wengi kwa kivuli chake tu .

Mfalme Herode Agripa I alipomuua Yakobo na kumfunga Petro ili kumuua pia, alitolewa gerezani kimuujiza akahama Yerusalemu (mwaka 44 hivi).

Katika Waraka kwa Wagalatia Paulo aliandika jinsi alivyomlaumu Petro wakiwa Antiokia kwa sababu ya kuficha msimamo wake wa kweli juu ya mahusiano na Wakristo wenye asili ya mataifa ili kuridhisha wale wenye asili ya Uyahudi.

Pia Paulo alimtaja katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho kama mtu mwenye wafuasi kati yao. Hivyo inaonekana alihubiri huko.

Waraka wa kwanza wa Petro unasema aliuandika akiwa Babuloni, jina la fumbo lililotumiwa na Wakristo kudokezea Roma. Kwa kuwa uliandikwa kwa Wakristo wachanga wa nyanda za juu za nchi inayoitwa leo Uturuki, inaonekana alikuwa amewahubiria kwanza.

Kifo chake

Yoh 21:18-19 inaeleza kifumbo kifodini ambacho Petro alimtukuza Mungu mjini Roma, katika mtaa wa Vatikano. Ndipo linapoheshimiwa kaburi lake chini ya altare kuu ya kanisa kubwa kuliko yote duniani.

Kifo hicho, inasemekana kwa kusulubiwa kichwa chini, miguu juu, kinashuhudiwa hasa na waandishi mbalimbali wa karne za kwanza, kama vile Papa Klementi I kati ya miaka 95 na 97, Ignasi wa Antiokia, Dionisi wa Korintho, Irenei wa Lyons, Klementi wa Aleksandria, Tertuliani, Jeromu n.k.

Vitabu vinavyomhusu

Mbali ya Barua ya kwanza, ambayo aliiandika mwenyewe kwa msaada wa Sila na kukubaliwa mapema kama kitabu kitakatifu, vitabu vingine viliandikwa kwa jina la Petro kuanzia mwisho wa karne ya 1.

Kati yake kimoja kimeingia katika Agano Jipya kama Waraka wa pili wa Petro, wakati vingine vyote vilikataliwa na Kanisa, kama vile Injili ya Petro, Matendo ya Petro na Ufunuo wa Petro.

Tazama pia

Tanbihi

Marejeo

  • Thenashara, Mitume Kumi na Wawili – tafsiri ya P. A. Bunju – Toleo la pili – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 1984 – ISBN 9976-63-030-1
  • Stefano Kaombe, Mfahamu Mtakatifu Petro anavyosimuliwa na Wainjili - Dar es Salaam 2017 - ISBN 9987-474-20-9

Viungo vya nje

Mtume Petro 
Wiki Commons ina media kuhusu:
Mtume Petro  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtume Petro kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Tags:

Mtume Petro Jina lakeMtume Petro Maisha yake ya awaliMtume Petro Baada ya kukutana na YesuMtume Petro Baada ya ufufuko wa YesuMtume Petro Kifo chakeMtume Petro Vitabu vinavyomhusuMtume Petro Tazama piaMtume Petro TanbihiMtume Petro MarejeoMtume Petro Viungo vya njeMtume PetroKarne ya 1MyahudiYesu Kristo

🔥 Trending searches on Wiki Kiswahili:

Amri KumiLatitudoWema SepetuAfrika ya MasharikiMbossoUongoziDalufnin (kundinyota)VitendawiliMtakatifu PauloIsimuUlayaHoma ya matumboUkatiliPaul MakondaBahari ya HindiHistoria ya IranKondomu ya kikeMisemoKoroshoMwanaumeSwalaJava (lugha ya programu)Barua rasmiUpendoMazungumzoUkristoOrodha ya kampuni za TanzaniaMaktabaVielezi vya mahaliMkoa wa MorogoroMofimuKigoma-UjijiBonde la Ufa la Afrika ya MasharikiNgano (hadithi)Virusi vya CoronaZuchuBongo FlavaDamuKidole cha kati cha kandoMwanzo (Biblia)DawatiNdoaKonsonantiVivumishi vya kuoneshaUzazi wa mpango kwa njia asiliaMapambano kati ya Israeli na PalestinaTreniSayansi ya jamiiTupac ShakurBendera ya TanzaniaShahawaUDAMauaji ya kimbari ya RwandaBurundiMbuga za Taifa la TanzaniaJokofuMuundoMkoa wa KataviUjimaUkristo nchini TanzaniaClatous ChamaDuniaNgiriMkoa wa MaraIsraelKipindupinduFananiShairiPumuJinsiaCristiano RonaldoOrodha ya Magavana wa Tanganyika🡆 More