Wachagga: Kabila la Kenya na Tanzania

Wachagga ni kabila la watu wenye asili ya Kibantu (lakini pia mchanganyiko wa damu, hasa ya Kikushi) wanaoishi kaskazini mwa Tanzania chini ya mlima Kilimanjaro, mkoani Kilimanjaro.

Wachagga: Vikundi vya Wachagga, Lugha ya Kichagga, Koo za Kichagga
Nyumba ya asili huko Marangu.

Wachagga ni kabila la tatu kwa ukubwa nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2003 zinaonyesha kuwa idadi yao ni watu 2,000,000. Hata hivyo kabila hilo ni kama mchanganyiko wa makabila madogomadogo yenye lugha tofauti, jambo la pekee nchini Tanzania.

Shughuli kubwa ya Wachagga ni biashara, kilimo na kazi za ofisini.

Vikundi vya Wachagga

Wachagga wana historia ndefu ya asili yao na ya maingiliano yao na makabila mengine. Kabila la Kichagga ni mkusanyiko wa makabila madogomadogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia mashariki (Tarakea, Rombo) hadi magharibi kwa Kilimanjaro (Siha, Machame).

Wachaga ni kama vile Wa-Vunjo ambao wanajumuisha watu wa Mwika, Mamba, Marangu, Kilema na Kirua ambayo ndiyo inajulikana na wengi kama Kirua Vunjo. Ukipenda unaweza kuwagawa watu hawa wa Vunjo kufuatana na vijiji hivyo. Wengine ni Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, Wa-Machame, Wa-Uru, na Wa-Siha.

Lugha ya Kichagga

Lugha ya Kichagga inabadilika kuanzia unapotoka Tarakea mpaka unapofika Siha magharibi mlima Kilimanjaro.

Kutokana na tofauti hizo Kichagga kimegawanyika katika Kirombo (ambacho nacho kinatofautiana kadiri unavyotoka eneo moja hadi jingine; mfano Kiseri, Kimashati, Kimkuu, Kimengwe, Kimahida), Kimachame, Kivunjo, Kimarangu, Kioldimoshi, Kingassa, Kiuru, Kikibosho, na Kisiha.

Lugha hizo zinakaribia kufanana kadiri makundi hayo yalivyopakana. Kwa mfano, Kivunjo kinafanana na Kioldimoshi. Vile vile Kisiha kinafanana sana na Kimachame ambacho pia kinafanana kidogo na Kikibosho.

Baadhi ya Wamachame walihamia sehemu za Meru, Arusha, na kuchanganyikana na Waarusha, hivyo lugha yao ikabadilika kidogo na kuwa Kimeru. Kwa sababu hiyo Wameru wanasikilizana sana na Wamachame ingawa lafudhi zao zinatofautiana kidogo.

Koo za Kichagga

Majina ya kiukoo ya Kichagga pia huashiria wanatoka sehemu gani ya Uchaga, japo si lazima kuwa hivyo: kwa mfano, familia maarufu za Kichagga nchini Tanzania ni kama ukoo wa akina Mushi au Moshi, Mmasy, Kimaro, Swai, Massawe, Lema, Urassa, Nkya, Ndosi, Meena n.k.

Akina Temu, Mlaki, Mlay, Lyimo, Moshiro, Mselle, Kamnde, Kileo, Tesha, Msaki, Assey, Kisaka, Mallya, Maembe, Shayo, Kessy, Ndanu, Macha, Mbishi, Moshi, Kombe, Njau, Mlingi, Chaky, Samky, Macha na Kilawe wanatoka Vunjo.

Majina mengine ya Old Moshi ni kama yafuatayo: Saria, Mmari, Macha, Machange, Mshiu, Kyara, Moshi, Massamu, Kimambo, Mboro, Mlngu, Saule, Tenga, Njau, Malisa, Maro, Maeda, Ringo,Olomi, Ngowi, Lyatuu na mengine mengi.

Kavishe, Mrosso, Bongole, Mariki, Moshi, Tarimo, Laswai, Mallya, Mrema, Mkenda, Mushi, Massawe, Silayo, Lyaruu, Makyao, Mowo, Lamtey, Tairo, Masue, Maleto, Mramba, Kauki, Kiwango na Kyauke wanatoka Rombo.

Mchaki, Masawe, Sawe, Usiri, Shayo, Kiwelu, Makundi, Urasa, Mtui, Moshi, Meela, Minja, Njau, Saria, Mtei wanatoka Marangu na Kilema.

Rite, Makule, Minja, Mashayo, Chao, Shao, Makawia, Ndesano, Kimario, Tilla, Mariale, Tarimo, Mafole, Kituo, Mrosso, Lyakundia, Kessy, Mmbando, Matemba, Ndenshau, Morio, Akaro, Matowo, Towo, Mkony, Temba, Foya, Munishi, Kilawe, na kadhalika hutoka Kibosho.

Ukoo wa akina Teri wako Mamba, Chami, Chuwa, Kiria Owoya na wachache Sango, Old Moshi na wengine walihamia Maji ya Chai, Mkoa wa Arusha.

Utawala wa jadi wa Wachagga

Watawala wa Kichagga waliitwa "Mangi". Akina mangi walihodhi mashamba, ng'ombe na waliheshimiwa kama viongozi wa jadi. Walikuwa na nguvu za kisiasa na utajiri. Baadhi ya Ma-mangi mashuhuri katika historia ni kama Mangi Shangali (wa ukoo wa Mushi) kutoka Machame, Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (Wajerumani), Mangi Sina wa Kibosho na Mangi Horombo wa Keni - waliojulikana kwa uhodari wao wa vita katika kupigana na Wamachame na kupora ng'ombe na mazao yao, na Mangi Marealle wa Marangu na Vunjo. Mangi Meli alikuwa mangi wa Waoldmoshi ambaye alipigana na Wajerumani na aliishia kukatwa kichwa; mpaka sasa fuvu lake lipo Ujerumani, alizikwa kiwiliwili tu baada ya kunyongwa; mti aliyonyongewa upo mpaka sasa sehemu ya Oldmoshi bomani karibu na Kolila Sekondari. Alinyongwa kwa sababu alikataa kuwa kibaraka wa kutumika na Wajerumani.

Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na viongozi hao wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia ndugu na watoto wa Ma-mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika serikali za kwanza. Hao pia wanaaminika walikuwa kama mabepari wa kwanza wa kijadi, maana walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao wamekaa kuhesabu mali zao. Hii ni desturi ya watawala, hasa wafalme kote ulimwenguni.

Elimu kati ya Wachagga

Wachagga wanajulikana kwa uwezo wao mkubwa katika uwanja wa elimu, hususani katika masomo ya sayansi na hisabati. Moshi ni maeneo ya mwanzo ambayo wamisionari wa Ukristo walijenga makanisa na shule.

Sababu hii imefanya Wachagga kuwa kabila namba moja lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa (elimu ya juu) na mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania. Kulingana na takwimu za elimu mkoa huo una shule za sekondari zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.

Shule nyingi za sekondari ziko katika mkoa huu kwa sababu zifuatazo:

  1. Hali ya hewa na vivutio vya kitalii katika mkoa huu viliwavutia zaidi walowezi na wakoloni na kuweka makazi yao hapo. Hivyo wamisionari walijenga shule za kwanza wakifuatiliwa na serikali za wakoloni
  2. Serikali ya Tanzania ilirithi shule zilizojengwa na wakoloni
  3. Wachagga waliobahatika kupata fedha binafsi baadaye waliwekeza kwenye ujenzi wa shule binafsi kama kitega-uchumi, wakati wakazi wa mikoa mingine kadhaa walisubiri serikali iwajengee shule.
  4. Ukichanganya sababu 1, 2 & 3 utagundua shule katika mkoa Kilimanjaro zimezidi sana idadi ya shule katika mikoa mingine yote.

Ni vema pia kusema kuwa shule hizo huvutia wanafunzi kutoka Tanzania nzima, haziwasomeshi Wachagga tu.

Ardhi

Ingawa ardhi ni msingi wa maendeleo kwa watu wote, kwa Wachagga, ardhi ni mali sana kwa sababu kilimo chao ni cha mazao ya kudumu kama kahawa na ndizi hukaa shambani kwa muda wa miaka mingi.

Mojawapo ya urithi wapewayo watoto ni "kihamba". Hii ni sehemu ya ardhi ambayo mtoto anategemewa atajenga na kuanzisha familia yake. Bahati mbaya watoto wa kike walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawanaji wa vihamba. Uhaba wa ardhi huko Uchaga ulipelekea Wachagga wengi kuhamia mikoa mingine. Hivi leo utakuta Wachagga wakiishi Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya n.k. wakiwa wamepanda migomba yao na kuendesha biashara za maduka ya vyakula, pamoja na biashara nyingine.

Ukienda kwenye mikoa hiyo utakuta wamejenga jamii zao na vyama vyao vya kusaidiana wakati wa sherehe au matatizo. Aidha hata pombe ya mbege utaweza kuikuta kwenye makusanyiko ya Wachagga katika mikoa mbalimbali.

Kilimo na chakula

Wachagga: Vikundi vya Wachagga, Lugha ya Kichagga, Koo za Kichagga 
Chakula cha Wachagga.

Wachagga hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, viazi, ndizi, ulezi na mboga mbalimbali. Pia mazao ya biashara kama vile kahawa, nyanya na vitunguu.

Ndizi za Wachagga na upishi wa samaki

Ingawa Wachagga wa leo wanakula vyakula mbalimbali kama vile ugali, wali na viazi, chakula kikuu cha Wachagga ni ndizi.

Kuna ndizi za aina mbalimbali na kwa matumizi tofauti. Mfano ndizi sukari ni fupi na huachwa hadi ziive na huliwa mbivu kama tunda.

Ndizi mshale hukatwa zikiwa mbichi na kupikiwa vyakula mbalimbali pamoja na nyama ya ng'ombe, kondoo au mbuzi. Mara nyingine hupikwa na maharage, choroko, kunde au hata maziwa ya mtindi. Vyakula vya ndizi huja kwa ladha tofauti kama vile ndizi nyama, mtori, machalari, kiburu na kadhalika.

Aina nyingine ni ndizi ng'ombe ambazo huachwa ziive halafu humenywa na kutumiwa kutengenezea kinywaji maarufu kiitwacho mbege. Mbege hutengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, maji, na ulezi.

Aina nyingine ni ndizi mzuzu. Hizi zikikomaa huachwa zianze kuiva kidogo halafu huchomwa na kuliwa kama kitafunwa pamoja na chai au kinywaji kingine. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam utaona ndizi mzuzu zikichomwa sambamba na muhogo au kuku vumbi au kiti moto.

Wachagga na muhogo

Inasemekana kuwa "Mchagga halisi hali muhogo - akila muhogo atakufa". Usemi huu umetokana na historia ya mababu kuwa Wachagga waliopanda mihogo Kilimanjaro enzi za kale walikufa baada ya kuila. Historia hiyo yaweza kuwa ya ukweli kwa sababu aina nyingi za mihogo zinajenga sumu ya sianidi ndani yake; watu waliozoea kutumia mihogo huwa na njia za kuondoa sumu kwa kuiloweka mihogo katika maji kwa muda. Lakini kama Wachagga wale wa zamani, hasa wa Machame, walifanya jaribio bila kujua mbinu ya kuondoa sumu, ajali iliweza kutokea. Cha kushangaza ni kwamba hukohuko Kilimanjaro, majirani na watani wa Wachagga, yaani Wapare, walikuwa wameshazoea mihogo na ilikuja kuwa moja ya chakula chao kikuu.

Ulaji kiti-moto

Pamoja na kilimo cha mazao, Wachagga hupendelea sana kufuga nguruwe kwa ajili ya biashara kwani nyama ya nguruwe hupendwa sana na watu na huuzwa sana kwenye baa na hoteli mbalimbali mijini hasa katika jiji la Dar es Salaam. Tabia ya kula nyama ya nguruwe ijulikanayo leo kwa jina la "kiti moto" ni moja ya mambo yaliyoenezwa na Wachagga. Ulaji wa "kiti moto" haukuwapendeza baadhi ya wenyeji wa Pwani na Dar es Salaam ambapo Wachagga walihamia, kwani wengi wao ni Waislamu, kwa hiyo nguruwe kwao ni haramu. Wakazi wa Dar es Salaam watokao makabila mengine na wasio Waislamu kwao kula nguruwe ilikuwa "ruksa".

Maoni juu ya Wachagga

Kipato cha Wachagga ni kikubwa kulingana na cha makabila mengine.

Wanawake wa Kichagga (hasa kutoka Machame) hujulikana kama wafanyakazi hodari. Huchangia sana katika mapato ya nyumbani na chakula. Mama wa Kichagga anaweza kushinda shambani kutwa na hana desturi ya kubeba watoto mgongoni kwenda nao shambani, hivyo wanakuwa nyumbani na mayaya au peke yao. Mfano ulio dhahiri ni nyakati za asubuhi na mapema kwenye vyombo vya usafiri karibu robo tatu ya abiria ni wanawake wakienda katika shuguli za biashara na kilimo na vivyo hivyo nyakati za jioni wakirudi majumbani. Hao ni nje ya wale wanaotumia usafiri wa miguu ambao ni wengi zaidi.

Ingawa wanaume wa Kichagga hupendelea kufanya kazi mbali na kwao, wake zao hukaa nyumbani (Kilimanjaro) kufuga ng'ombe na kufanya kazi za shambani. Kwa sasa kutokana na ugonjwa wa ukimwi tabia hii imepungua miongoni mwao.

Pia baadhi ya kina mama wa Kichaga wanawajali waume zao zaidi kwani nyama nzuri ni ya baba. Ili kuepuka gharama baba ataandaliwa chakula kizuri, tofauti na chakula walichoandaliwa watoto, japo ni chakula kilekile.

Pia Wachagga wamekuwa na desturi ya kuwaenzi wazee wao waliotangulia mbele za haki kwa kuwatambikia kwa pombe na nyama za mbuzi pale tu wanaporudi nyumbani mwezi Desemba. Hilo limekuwa suala la kawaida sana. Wengi wao huwa wanarudi na magari, ndiyo sababu utaona ya kwamba kila mwaka ufikapo mwezi Desemba foleni za magari zimekuwa zikiongezeka katika mji wa Moshi kutokana na Wachagga kurudi nyumbani msimu wa sikukuu. Wengi wao wamekuwa wakitoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.

Wachagga wengi hupenda kurudi nyumbani kipindi cha Krismasi, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu. Pia imekuwa kama desturi wanaukoo kukaa pamoja na kujadiliana mambo jinsi yalivyokwenda katika kipindi kizima cha mwaka na wakati mwingine inakuwa sehemu ya kwenda kuwatambulisha watoto kwa bibi na babu zao, hasa wale waliozaliwa mijini. Ni kipindi chenye shangwe na furaha sana: hakuna kaya utakayokuta haina furaha kwa sababu hata kama huna sherehe kuna mialiko mbalimbali ambao haihitaji kadi au michango.

Ingawa wengi hudhani kwamba Wachagga wamepokea sana dini (imani) ya Ukristo kwa kuwa wengi wao ni Wakristo na hiki huwa kipindi cha likizo kwao, inaaminika pia kuwa kurudi kwao wakati wa Krismasi ni pamoja na kutembelea ndugu zao na kujumuika pamoja katika kuumaliza mwaka baada ya kazi nyingi za kutafuta pesa mwaka mzima.

Sababu kuu za Wachaga wengi kwenda kwao mwisho wa mwaka

  1. Kupumzika, hii ni baada ya kufanya kazi kwa mwaka mzima bila kwenda, biashara asubuhi, jioni mahesabu, kwao Desemba ni mwezi wa kutulia tu na familia ndugu na jamaa
  2. Kuchinja mbuzi, hapa kuna za matambiko na za kula na kufurahia tu. Matambiko hayo ni kushukuru wazee wao waliokufa mapema kwa baraka walizopata kwa kipindi chote cha mwaka mzima
  3. Sherehe mbalimbali: sherehe za wafu, maadhimisho ya ndoa mbalimbali, Krismasi, Ubatizo, Kipaimara, Komunyo, kutoa watoto jandoni na Mwaka mpya wenyewe. Kila inayoitwa sherehe hufanyika kipindi hiki, kuanzia tarehe 25 Desemba kufika tarehe 1 Januari ni shughuli tu, kula kunywa kusaza.
  4. Utambulisho mbalimbali kwa wazee, jamaa wa nyumbani kama vile mke, mchumba, mume, gari jipya, nyumba mpya, watoto n.k.
  5. Kukutana na watu mbalimbali ambao hamuonani baada ya kipindi hicho kama, marafiki, majirani, ndugu na jamaa. Hii ni kwa wale wanaofanya kazi mikoa tofauti (huyu Morogoro yule Mwanza mwingine katoka Dar es Salaam)
  6. Utekelezaji wa miradi mbalimbali hapo nyumbani kama ujenzi au ukarabati wa nyumba, njia pana za magari na kukagua mashamba n.k.

Si wote wanakwenda kwa sababu hizo zote bali lazima sababu mojawapo ihusike.

Kutokana na sababu hizo wanaokwenda ni watu wote wa dini zote. Ukienda tofauti na kipindi hiki huwezi kukuta watu wengi sana. Kwanza baada ya kipindi hicho kupita kila mtu anashughulika na mambo yake (kutafuta pesa).

Kama umekwenda na huna chochote, utakumbana na ubaguzi na manyanyaso makubwa.

Tanbihi

Marejeo

  • Ehret, Christopher (2002). The Civilizations of Africa. University of Virginia Press. ISBN 0-8139-2085-X. 
  • Gray, R (1975). The Cambridge History of Africa. Cambridge University Press. ISBN 0-521-20413-5. 
  • Fasi, M El (1992). Africa from the Seventh to the Eleventh Century. University of California Press. ISBN 0-520-06698-7. 
  • Johnson, H.H (1886). "Copyright: Tubner & Co". Journal of the Royal Anthropological Institute of Great Britain and Ireland XV: 12–14. 
  • Yakan, Mohamad A (1999). Almanac of African Peoples & Nations. Transaction Publishers. ISBN 1-56000-433-9. 
  • P. H. Gulliver (1969). Tradition and Transition in East Africa: Studies of the Tribal Element in the Modern Era. University of California Berkeley. 

Viungo vya nje

Wachagga: Vikundi vya Wachagga, Lugha ya Kichagga, Koo za Kichagga  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wachagga kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Tags:

Wachagga Vikundi vya Wachagga Lugha ya KichaggaWachagga Koo za KichaggaWachagga Utawala wa jadi wa Wachagga Elimu kati ya Wachagga ArdhiWachagga Kilimo na chakulaWachagga Maoni juu ya Wachagga TanbihiWachagga MarejeoWachagga Viungo vya njeWachaggaAsiliDamuKabilaKaskaziniKibantuKikushiMkoa wa KilimanjaroMlimaMlima wa KilimanjaroTanzaniaWatu

🔥 Trending searches on Wiki Kiswahili:

NduniDiniUkimwiUenezi wa KiswahiliFani (fasihi)MizimuBahashaUtohoziMofolojiaHistoria ya BurundiMwanamkeVidonge vya majiraMkutano wa Berlin wa 1885HeshimaViwakilishi vya pekeeBagamoyo (mji)MweziJKT TanzaniaKibodiUzalendoMajira ya baridiAlama ya uakifishajiFonimuPichaJohn Raphael BoccoMvuaDivaiAina za ufahamuInsha ya wasifuJinaAfande SeleSteven KanumbaMuungano wa Madola ya AfrikaDamuTarakilishiMfumo wa mzunguko wa damuMakabila ya IsraeliMvua ya maweTeknolojiaRoho MtakatifuUkristoHomoniHafidh AmeirUzazi wa mpangoKitenzi kikuu kisaidiziMkoa wa NjombeWanyaturuInsha za hojaTawahudiGhanaOrodha ya nchi za Afrika kulingana na idadi ya watuIniMkoa wa MbeyaMjasiriamaliMagonjwa ya machoNomino za dhahaniaMjombaMachweoMariooPombooViungo vinavyosafisha mwiliVita ya Maji MajiOrodha ya nchi za Afrika kulingana na pato la taifaWilaya ya NyamaganaUmoja wa AfrikaMatumizi ya lugha ya KiswahiliMapenziMfumo wa upumuajiWilaya ya Unguja Magharibi ASilabiLigi ya Mabingwa Afrika🡆 More