Ujamaa ni siasa iliyoanzishwa kwa misingi ya sera za Julius Nyerere za maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi katika Tanzania punde tu baada ya Tanganyika kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1961.
Mwaka 1967 Rais Nyerere alichapisha mwongozo wa maendeleo yake, ambao uliitwa Azimio la Arusha, ambapo alionyesha haja ya kuwa na mtindo wa Kiafrika wa maendeleo; huo ukawa msingi wa Usoshalisti wa Afrika.
Ujamaa linatokana na neno la Kiswahili linalomaanisha familia au jamii na hujulikana kwa sifa kadhaa muhimu, yaani mtu anakuwa mtu kwa kupitia watu au jamii.
Nyerere alitumia Ujamaa kama msingi wa mradi wa maendeleo ya taifa. Aliitafsiri dhana ya Ujamaa kuwa mfumo wa usimamizi wa kisiasa na wa kiuchumi kwa namna mbalimbali:
Uongozi wa Julius Nyerere uliivutia Tanzania macho na heshima ya kimataifa kutokana na msisitizo wake wa maadili kama msingi wa maamuzi ya siasa. Chini ya Nyerere Tanzania ilipiga hatua kubwa katika vipengele mbalimbali vya maendeleo: vifo vya watoto vilipungua kutoka 138 kwa 1000 waliozaliwa hai mwaka 1965 hadi 110 mwaka 1985; tarajio la kuishi lilipanda kutoka miaka 37 (1960) hadi 52 (1984); uandikishaji wa wanafunzi katika shule ya msingi ulipanda kutoka 25% (16% tu kwa watoto wa kike) mwaka 1960 hadi 72% (85% kwa watoto wa kike) mwaka 1985 (ingawa idadi ya wananchi ilikuwa inaongezeka kwa kasi); asilimia ya watu wazima waliojua kusoma na kuandika ilipanda kutoka 17% mwaka 1960 hadi 63% mwaka 1975 (juu sana kuliko nchi nyingine za Afrika) ikaendelea kupanda.
Hata hivyo Ujamaa (kama vile mipango mingine ya uzalishaji wa pamoja) ulipunguza uzalishaji hata kutia shaka juu ya uwezo wake wa kustawisha uchumi.
Hatimaye sababu mbalimbali zilifanya Ujamaa uonekane umeshindikana kiuchumi. Kati ya hizo, tatizo la kimataifa la mafuta miaka ya 1970, anguko la bei ya bidhaa zilizozalishwa nchini (hasa kahawa na katani), utovu wa uwekezaji kutoka nje ya nchi na vita vya Uganda-Tanzania miaka 1978-1979 vilivyofyonza sana mtaji muhimu, na miaka miwili mfululizo ya ukame.
Kufikia mwaka 1985 ilikuwa wazi kwamba Ujamaa ulishindwa kutoa Tanzania nje ya ufukara wake; Nyerere alitangaza kuwa atang'atuka asigombee tena urais katika uchaguzi wa mwaka huohuo.
Ujamaa ulivunjwa (ingawa si kinadharia) mwaka 1985 wakati Nyerere alipomwachia mamlaka Ali Hassan Mwinyi aliyeingiza nchi katika taratibu za soko huria.
Nyerere alitumia Sheria ya Kuzuia Kutiwa Nguvuni bila sababu kukandamiza vyama vya wafanyakazi na kuwakamata wapinzani kikatili kupindukia; walioathiriwa huhesabiwa kuwa maelfu.
Mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International yalipiga kampeni dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania.
Vyombo vya habari nchini vilidhibitiwa kwa kunyimwa usajili rasmi.
Serikali iliwalazimishwa watu kuhamia mashamba ya pamoja, jambo ambalo lilitatiza shughuli za kilimo na uzalishaji.
Wengine walilazimishwa, kwa mfano, kwa kuchoma vijiji vyao. Nyumba ziliteketezwa kwa moto au kubomolewa, wakati mwingine pamoja na mali ambayo familia hizo zilikuwa nayo kabla ya Ujamaa.
Watu walipoteza heshima kwa utamaduni na maeneo kama vile makaburi ya mababu zao.
Polisi na wanajeshi waliojihami kwa silaha walitumika katika uhamisho wa watu. Tanzania iligeuka kutoka taifa la wakulima waliojitahidi kukidhi mahitaji yao na kuwa taifa la wakulima walioangamia kwa njaa kwa pamoja.
Taifa lilinusurika kwa kutegemea msaada ya kigeni ya chakula ambacho walipewa tu watu waliokubali kujiunga na Ujamaa.
Serikali iliwapa ahadi ambazo baadaye ziligeuka kuwa uongo.
Uchumi ulianguka. Kiasi kikubwa cha utajiri wa nchi aina ya mijengo na kuboresha miundo ya ardhi (mashamba, miti ya matunda, nyua) iliharibiwa au kutelekezwa kwa lazima .
Mifugo waliibwa, kupotea, kupata magonjwa, au kufa.
Suleman Sumra aligundua kuwa mavuno katika mashamba ya Ujamaa kwa pamoja yalikuwa chini kwa asilimia 33-85 kuliko yale ya mashamba yaliyomilikiwa kibinafsi. Kwa wastani yalikuwa chini kwa asilimia 60. Wakulima wa pamoja hawakuwa na motisha za kufanya kazi.
Hali ya nchi ilienea haraka na kuathiri karibu kila sekta. Mwaka 1967, ustawishaji wa taifa ulibadilisha serikali na kuifanya mwajiri mkubwa zaidi katika nchi. Ilihusika katika kila kitu, kuanzia kufanya mauzo ya rejareja hadi biashara ya kuuza na kuagiza bidhaa kutoka ng'ambo na hata uokaji, na kuleta mazingira muafaka kwa ufisadi.
Ukiritimba na taratibu zisizoeleweka ziliongezeka na viwango vya juu vya kodi kuwekwa.
Fedha za umma zilitumika vibaya na kuweka kwa matumizi yasiyo na faida. Uwezo wa kununua ulipungua kwa kiwango kikubwa mno na hata bidhaa muhimu zikawa hazipatikani.
Mfumo wa kutoa vibali uliwaruhu maafisa wakuu kuchukua rushwa kubwa ili kutoa vibali. Msingi wa mfumo wa ufisadi ukawa umewekwa.
Barabara ziliharibika na kuwa kati ya barabara mbovu zaidi barani Afrika.
Sekta ya viwanda ikadidimia. Kampuni ya mgodi iliyomilikiwa na serikali ikaonekana kushindwa.
Benki ya Dunia pia imekosolewa kwa kuchangia mpango huo: "Nchini Tanzania, kwa mfano, Benki hii ilitoa fedha kwa kampeni ya udikteta wa Julius Nyerere unaoitwa Ujamaa, ni mfano wa mfumo wa vijiji wa Mengistu. Wakulima walipoteza uhuru wao, na nchi ilichukua ardhi yao na kudai mazao yao, yote haya kwa msaada na baraka za Benki ya Dunia. Katika miaka michache tu, Nyerere aligeuza nchi yake kuwa gofu, taifa la waombaji. Lakini Benki hii haijawahi kukubali makosa haya.
Muziki wa hip hop nchini Tanzania ulipata msukumo kutokana na mawazo na mandhari ya Ujamaa. Mwaka 1967, baada ya Rais Nyerere kuanzisha itikadi mpya ya siasa, ambayo aliahidi itawakomboa Watanzania kutoka ubeberu wa kimataifa, ilitelekezwa na wanasiasa wa Tanzania, kanuni za Ujamaa zilifufuliwa tena kupitia "njia isiyotarajiwa: Wanamuziki wa Rap na wasanii wa hip hop katika mitaa ya Tanzania.
Kama jawabu kwa miaka ya viongozi wafisadi wa serikali na wanasiasa baada ya Nyerere, dhana za umoja na familia na usawa zilikuwa ndio ujumbe uliotumwa katika muziki uliokuwa unatayarishwa. Hii ilikuwa kama mwitikio wa darasa la wafanyakazi katika mtazamo fulani ilikuwa upinzani.Kanuni za uchumi wa ushirika -"wananchi wa kawaida kushirikiana ili kujipatia mahitaji muhimu ya maisha" - ni maneno yanayoweza kuonekana katika nyimbo nyingi za hip hop za wasanii wa Tanzania. Zinapigia upatu ukuzaji wa biashara na kujitegemea katika jitihada za kuinua mioyo ya vijana na kuhamasisha mabadiliko katika jamii.
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Ujamaa, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.