Maafa asilia ni matukio yanayosababisha mabadiliko kwenye uso wa ardhi au angahewa ya dunia yanayoleta hasara kubwa kwa mali na maisha ya binadamu, na sababu zake ni za kiasili.
Mifano yake ni tetemeko la ardhi, banguko, kimbunga, mafuriko, tsunami, mlipuko wa volkeno au pigo la asteroidi. Matukio hayo yote si lazima yawe maafa kwa maana yakitokea mahali pasipo na wanadamu na kutosababisha hasara kwa watu basi hayaitwi "maafa".
Kuna maafa mbalimbali yanayosababishwa na binadamu na sababu za kibinadamu huingiliana na maafa asilia:
Mara nyingi ni matendo ya binadamu yanayofanya tukio la kiasili kuwa maafa makubwa kwa mfano ujenzi wa makazi katika mazingira ya volkeno hai (mfano: mji wa Napoli, Italia kando ya Vesuvio) au penye mipaka ya mabamba ya gandunia inayojulikana kama vile Los Angeles, Marekani.
Tetemeko la ardhi (pia: zilizala) ni mishtuko ya ghafla kwenye ganda la dunia. Likifikia ukali fulani ni hatari hasa kwa majengo. Hatari kwa binadamu hutegemea ubora wa majengo. Vifo vingi vinaweza kutokea wakati majengo yanaporomoka na kujeruhi au kuua watu. Hata tetemeko kali haliui watu waliopo porini katika tambarare ingawa linatisha.
Nguvu ya tetemeko la ardhi hupimwa kwenye skeli ya 0-9 au zaidi.
Nguvu ya uharibifu inaweza kutofautiana sana. Kwa mfano, tetemeko la ardhi lenye nguvu ya 6.4 liliharibu mji wa Bam, Iran mwaka 2003 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40,000. Lakini tetemeko huko Northridge, Kalifornia ya mwaka 1994 ilikuwa na nguvu ileile ila ni watu 60 tu waliofariki. Tofauti ilikuwa ubora wa majengo katika maeneo yaliyohusika. Ilhali takriban wanafunzi 10,000 walifariki, huko Marekani shule zote zilisimama. Athira nyingine ilikuwa hali ya huduma za dharura na muda wa mahanga kukaa chini ya kifusi cha majengo.
Banguko ni kiasi kikubwa cha mawe, ardhi, theluji au barafu kinachoanza kuteleza kwenye mtelemko wa mlimani na kuelekea bondeni. Banguko unaweza kusababishwa na tetemeko la ardhi, kuyeyuka kwa theluji mlimani au mvua kali.
Banguko kubwa la mwaka 1999 nchini Venezuela liliharibu nyumba zaidi ya 8,000 na kuua idadi ya watu isiyojulikana lakini imekadiriwa kuwa kati ya watu 10,000 hadi 30,000. Mwaka 2010 banguko kwenye mitelemko ya mlima Elgon huko Uganda likaua watu zaidi ya 100.
Tufani na kimbunga ni aina za dhoruba zenye mwendo wa kuzunguka. Zinatokea hasa katika kanda la tropiki la dunia. Zinaleta upepo mkali mno pamoja na kiasi kikubwa cha mvua. Zinaweza kubomoa nyumba, kuvuta watu na hata magari hewani na kuleta mafuriko makali.
Tufani ya Katrina ya mwaka 2005 iliharibu mji wa New Orleans huko Marekani, ikasabisha vifo zaidi ya 1,200 na hasara ya mali ya takriban dolar za Marekani bilioni 108 .
Mafuriko ni hali ya kuwa na maji mengi yanayofunika nchi kavu isiyo na maji kwa kawaida.
Mafuriko yanaweza kutokea
Mafuriko mara nyingi ni hatari kwa binadamu, huleta hatari kwa uhai, mali na nyumba.
Njia za kujiokoa ni pamoja na kuhama haraka sehemu za mabondeni kwenda penye miinuko au nchi ya juu zaidi. Watu waliozoea mafuriko wana mbinu za pekee kama vile kujenga vizuizi vya maji kupanda juu, kuchimba mifereji inayopeleka maji mbali au kujenga nyumba juu ya vilima wakijua hakuna njia ya kuzuia mafuriko.
Tsunami ni wimbi kubwa sana katika bahari inayosababishwa na tetemeko la ardhi, mlipuko wa volkeno au matokeo mengine yanayoleta mshtuko wa ghafla chini ya maji. Mshtuko huo unapita ndani ya maji si hatari sana kwa meli baharini maana haubadilishi mno uso wa bahari. Lakini pale unapokutana na nchi kavu au kufikia sehemu ambako kina cha maji kinapungua kuna wimbi kubwa linalotokea na hii ni hatari kwenye pwani ambako wimbi hilo linafikia.
Tsunami inaweza kutokea pia baada ya banguko la mtelemko mkubwa kwenye pwani ya bahari au ziwa. Kabla ya kipindi cha kihistoria kulikuwa pia na tsunami zilizosababishwa na mgongano wa gimba la angani na uso wa dunia.
Tsunami zimewahi kutokea mara nyingi duniani. Kati ya taarifa za kwanza zilizotambua uhusiano kati ya tetemeko la ardhi na tsunami ni mwandishi Thukidides wa Ugiriki ya Kale mnamo mwaka 426 KK.
Tsunami kubwa iliyotazamwa kwa msaada wa vifaa vya kisayansi ni Tsunami wa Krismasi 2004 katika Bahari Hindi iliyoua maelfu ya watu kuanzia Indonesia, Sri Lanka, Thailand na India hadi Somalia na Kenya. Ilisababishwa na tetemeko la ardhi kutokana na mwendo wa mabamba ya gandunia, hapa bamba la Burma chini ya bamba la Uhindi.
Mlipuko wa volkeno ni kutokea vikali kwa lava na gesi kutoka ndani ya ganda la dunia. Volkeno hupatikana pale ambako vipande vya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Kuna pengo ambako magma joto kutoka ndani ya dunia inapanda juu kufika usoni.
Hii inaweza kutokea polepole lakini ikitokea kwa ghafla inaleta maafa katika mazingira yenye makazi ya watu.
Milipuko ya volkeno mbalimbali zinaweza kutofautiana kutegemeana na aina ya volkeno na hasa aina ya magma na lava zinazotoka nje.
Dunia yetu inazunguka Jua letu katika anga-nje. Hapa inakutana mara kwa mara na violwa vinavyoanguka kwenye angahewa na kuonekana kama vimondo. Vingi ni vidogo, hivyo havileti hasara.
Lakini kiolwa kinachogonga Dunia kikiwa kikubwa kama asteroidi hatari ni kubwa. Migongano hiyo hutokea mara chache sana lakini sayansi imetambua ya kwamba pigo la asteroidi kubwa miaka milioni 66 iliyopita lilisababisha kuangamia kwa spishi nyingi, zikiwa pamoja na dinosauri. Pigo hilo lilirusha kiasi kikubwa cha vumbi kwenye angahewa pamoja na kusababisha milipuko ya volkeno nyingi na kuleta mabadiliko ya tabianchi kwa miaka kadhaa, hivyo kushusha halijoto duniani na kusababisha giza kwa muda mrefu.
Katika karne iliyopita kulikuwa na matukio mawili yaliyoonyesha nguvu haribifu ya violwa kutoka anga-nje:
Kutambuliwa kwa hatari hii imesababisha mataifa mbalimbali kushirikiana katika mipango ya kutambua mapema violwa vinavyokaribia Dunia.
Makala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Maafa asilia, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.