Kamusi za Kiswahili ni zile zinazofafanua maana ya maneno ya lugha hiyo ya Afrika Mashariki ambayo inazidi kuenea hasa barani Afrika.
Kamusi hizo ni vyombo muhimu kwa kukuza na kuimarisha Kiswahili, ambacho kwa sasa ni lugha rasmi ya Jumuia ya Afrika Mashariki na mojawapo kati ya lugha za mawasiliano za Umoja wa Afrika.
Kamusi za lugha hiyo zilianza kupatikana katika karne ya 19 BK, kabla na wakati wa ukoloni wa Kizungu katika nchi za Afrika Mashariki. Hivyo watungaji wa kamusi za kwanza walikuwa Wazungu waliofahamu vizuri lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, n.k.
Waswahili wenyewe, watu wa pwani ya Afrika Mashariki na visiwa vya jirani (kama Unguja na Pemba), hawajulikani kuwa wametunga kamusi kabla ya wakati huo. Wasomi wao walijua kwa viwango tofauti Kiarabu, ambacho kilikuwa lugha kuu ya elimu kwenye mwambao wa Bahari Hindi mashariki mwa Afrika na pia lugha ya kidini katika Uislamu.
Vilevile hatuna habari kwamba Wareno waliofika Afrika ya Mashariki tangu mwaka 1500 hivi walitunga kamusi.
Utungaji wa Kamusi za Kiswahili ulianza kwa kukusanya orodha za maneno/msamiati wa Kiingereza-Kiswahili na Kifaransa-Kiswahili. Msamiati wa Kiswahili ulikusanywa ili kuwasaidia wageni hawa kuifahamu lugha ya Kiswahili na waweze kuwasiliana na wenyeji wao ambao ni Waswahili. Nakala za msamiati huo zilipelekwa Uingereza ili wageni wengine waliotaka kufika Afrika Mashariki wajifunze kabla hawajafika katika nchi hizo.
Mfano wa kwanza ni mkusanyo wa maneno uliyofanywa na nahodha Mwingereza T. Smee alipotembelea pwani kuanzia Somalia hadi Zanzibar kwenye mwaka 1811-1812; alikusanya istilahi 250 hivi za Kiingereza na maana yake kwa Kiswahili (alichoita "Souallie"), Kisomali na lugha ya Wagalla. Orodha hiyo ilichapishwa kwenye mwaka 1844. Wengine wanaotajwa ni Henry Salt (1811-1813) na Browse Ross (1843). Msamiati uliokusanywa na watu hao unafikiriwa kuwa ni wa Kiswahili cha kaskazini mwa Mombasa na ulikuwa na maneno machache sana. Wakati huo mchungaji Krapf alikuwa ameshaanza kazi ya kutunga kamusi yake.
Kamusi ya kwanza inayojulikana ilitungwa mnamo 1848 na Ludwig Krapf huko Rabai Mpya / Mombasa (Kenya); ilikamilishwa na kutolewa kama "A Dictionary of the Suahili language, London 1882". Kamusi inapatikana pia mtandaoni.
Tahajia ya maneno mara nyingi ni tofauti na kawaida ya leo kwa sababu usanifishaji wa lugha ulitokea tu miaka 40-50 baada ya kutolewa kwa kamusi yake; pia alikusanya maneno mengi huko Rabai / Mombasa kwa hiyo athira ya Kimvita ni kubwa. Pia kuna changamoto kutumia kamusi yake kwa sababu ilhali alitoa maana ya maneno ya Kiswahili kwa Kiingereza aliongeza maelezo juu ya matumizi na etimolojia kwa lugha ya Kilatini.
Alipoanza kazi aliamua kutotumia mwandiko wa Kiarabu uliokuwa njia ya kawaida ya kuandika Kiswahili akiona haulingani sana na lugha yenyewe, maana Kiarabu kina herufi kadhaa kwa sauti ambazo hazipatikani katika Kiswahili. Alitafakari angetumia herufi za Kiamhari (alichojua vizuri) lakini aliamua kuendelea kwa alfabeti ya Kilatini kwa sababu hakutaka kuwapa wanafunzi wa lugha tatizo la kupambana na alfabeti ya ziada.
Wengine walioendelea kukusanya maneno na kutoa kamusi ni Askofu Edward Steere na mwanaisimu A.C. Madan. Wote wawili walifanya kazi Zanzibar wakiwa wamisionari wa Kanisa Anglikana.
Kamusi ya Kiswahili - Kijerumani ya kwanza ilitungwa mwaka 1890, wakati wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, na Carl Gotthilf Büttner (Wörterbuch der Suaheli-Sprache, Berlin 1891) aliyetoa pia matini za Kiswahili kwa mwandiko wa Kiarabu. Kamusi pana zaidi ilitolewa mwaka 1911 na Carl Velten (Suaheli Wörterbuch, Berlin 1910).
Kamusi ya Kiswahili - Kifaransa ilitolewa na Charles Sacleux (Sacleux, Charles. 1939. Dictionnaire Swahili - Français. (Travaux et Mémoires de l'Institut d'Ethnologie, Vols. 36/37). Paris: Institut d'Ethnologie, Université de Paris. (Reprint 1959). Sacleux alikuwa padre katika misheni ya Kikatoliki huko Bagamoyo. Kamusi hii imesifiwa kuwa ya pekee kwa jinsi iliyokusanya pia maneno ya lahaja za Kiswahili nje ya Kiunguja (Zanzibar) na Kimvita (Mombasa) na kwa upana wa maelezo yake kuhusu historia ya maneno.
Hadi mwanzo wa karne ya 20 Kiswahili kilipatikana katika lahaja zake tu. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza Uingereza ilitawala maeneo makuu ambako Kiswahili kilitumiwa. Hapo serikali ya kikoloni iliánzisha kamati kwa kusudi la kuunda Kiswahili sanifu kitakachotumiwa kote Afrika ya Mashariki. Kamusi mbili za "Inter-territorial Language (Swahili) committee to the East African Dependencies" zilitolewa mwaka 1939 na zimechapishwa upya mara nyingi. Mhariri mkuu wa kamati alikuwa katibu wake Frederick Johnson. Msingi wa kamusi hizi ulikuwa kazi ya Madan (taz. juu). Hivyo kamusi hizi hutajwa kama "Madan-Johnson".
Tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi za Afrika ya Mashariki Kiswahili kiliendelea sana. Azimio la serikali ya Tanzania la kufanya Kiswahili kuwa lugha ya elimu katika shule za msingi lilianzisha masharti ya kutunga vitabu vya shule na kupanua msamiati wa Kiswahili. Orodha za maneno zilitungwa kwa ajili ya masomo mbalimbali.
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (leo: TATAKI) katika Dar es Salaam ilianza kuandaa kamusi mbalimbali, hasa "Kamusi ya Kiswahili Sanifu" inayoeleza maana ya maneno kwa kutumia lugha yenyewe. Kamusi mbalimbali zilifuata.
Vifupisho katika mabano si vya kawaida lakini vimeingizwa hapa kwa kusudi la kurahisisha marejeo katika makala za Wiki Kiswahili.
M.A.J.E. CHIPA, Francais-Kiswahili-English / Misamiati ya msingi kwa wanaojifunza lugha Kifaransa-Kiswahili-Kiingereza - MAJEC-AJEJER, Dar es Salaam 2006, ISBN 9987 451 16 0
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Kamusi za Kiswahili, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.