Utawala wa Kijiji ni miongoni mwa tawala katika serikali za mitaa za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huu ni utawala wa chini kabisa kimuundo ukitanguliwa na utawala wa Kitongoji.
Kuwa utawala wa chini haimaanishi kuwa na umuhimu mdogo; isipokuwa ni kupitia utawala huu ndiko ambako mambo mengi yanayoamuliwa au kupangwa na tawala za juu kama serikali, hutekelezwa.
Utawala wa kijiji huelekeza wananchi katika kutumia madaraka yao ya kidemokrasia kuamua juu ya mambo yanayowahusu kama wanakijiji moja kwa moja bila kupitia mlolongo au urasimu mrefu.
Mambo yanayohusiana na tawala za serikali za mitaa yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kila mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana wajibu wa kupinga na kukataa kila aina ya uovu katika jamii vikiwemo rushwa, uonevu, wizi, ubadhirifu wa mali za umma na ya watu binafsi.
Pia ana jukumu la kudai na kupigania haki zake na za wananchi wengine, kutoa malalamiko na kuuliza maswali juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea kijijini au kwenye mtaa kupitia vyombo mbalimbali vya kijamii na kiserikali.
Wananchi wanashiriki katika serikali za mitaa kupitia vikao au mikutano mbalimbali ambapo hujadili na kutoa mapendekezo yao kuhusu mipango na matatizo yanayowakabili kwa namna moja au nyingine ili kuweza kupatiwa ufumbuzi na kurahisisha uboreshaji wa huduma za kijamii katika maeneo yao wanamoishi.
Hiki ni chombo kikuu kabisa cha utawala wa kijiji. Kijiji kipo kwa mujibu wa sheria. Wajumbe wa mkutano wa kijijii ni wanakijiji wote waliofikia umri usiopungua miaka 18. Hakuna akidi maalum, kila kijiji hujiwekea akidi yake; inayofaa ni kati ya 20% hadi 33%. Kwa kawaida mkutano hukutana kila baada ya miezi mitatu, kikao cha dharura kinaweza kuitishwa kukiwa na haja na kufanya hivyo, hata hivyo sheria haisemi nani anaita kikao cha dharura. Taarifa ya kuitisha Mkutano Mkuu wa kijiji/mtaa hutolewa kwa siku saba.
Kila baada ya miaka mitano kinakuwa na Mkutano Mkuu Maalum wa uchaguzi wa Mwenyekiti na wajumbe wa halmshauri ya Kijiji. Mkazi wa kijiji anayegombea nafasi ya uongozi kwenye halmashauri ya kijiji au uenyekiti wa kijiji lazima awe na umri usiopungua miaka 21. Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu ni Mwenyekiti wa kijiji akisaidiwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO). Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) hupanga ratiba za vikao, kuandaa na kuitisha vikao vya Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Halmashauri ya kijiji ni chombo kikuu cha utendaji katika utawala wa kijiji. Hukutana mara moja kila mwezi, mikutano ya dharura inaweza kuitishwa. Akidi (qorum) ya vikao vya halmshauri ya kijiji ni nusu ya wajumbe wote wa halmashauri ya kijiji. Wakati Mkutano Mkuu ni kama Bunge, halmshauri ya kijiji ni kama serikali. Huchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Uchaguzi wa halmashauri wa kijiji husimamiwa na Mkurugenzi wa halmshauri ya Wilaya. Mkazi wa kijiji mwenye umri usiopungua miaka 21 ana sifa za kuchaguliwa kwenye halmshauri ya kijiji. Wajumbe wa halmashauri ya kijiji wanatakiwa wasizidi 25 na wasiopungua 15. Mkutano Mkuu kwa kushirikiana na Msimamizi wa uchaguzi idadi ya wajumbe wanayotaka kutokana na mazingira yao kutegemea na wingi wa wakazi na ukubwa wa eneo lao (idadi ya vitongoji).
Wajumbe wa halmashauri ya kijiji ni Mwenyekiti wa kijiji, wenyeviti wa vitongoji, wanawake ambao watakuwa theluthi moja ya wajumbe wote na wajumbe wengine. Mwenyekiti wa kijiji ni mwenyekiti wa halmshauri ya kijiji na mwenyekiti wa Mkutano Mkuu. Wenyeviti wa vitongoji huchaguliwa na wakazi wa vitongoji huingia kwenye halmashauri ya kijiji kwa mujibu wa nyadhifa zao.
Ushiriki wa wananchi ni jambo la msingi sana katika kujiletea maendeleo yao katika vijiji na mitaa. Mahali ambapo wananchi hawashiri wala hawashirikishwi kunakuwa na lawama na mizozo mingi kwa viongozi hasa pale ambapo maamuzi yaliyopitishwa yanawaumiza wananchi. Hapa ndipo wengi huona umuhimu wa kushiriki unapojitokeza zaidi.
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Utawala wa Kijiji - Tanzania, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.