Gandunia (kutoka maneno ganda na dunia; en:plate tectonics) ni mafundisho ya sayansi za jiolojia na jiofizikia kuhusu tabia za ganda la dunia na miendo ya sehemu zake.
Inaanza na hoja ya kuwa muundo wa dunia ni wa tabaka mbalimbali. Tabaka imara ni ganda la nje la dunia pamoja na sehemu ya juu ya koti ya dunia chini ya ganda hilo. Tabaka hiyo -inayoitwa "tabakamwamba"- inakaa juu ya tabaka moto na laini.
Ndani ya tabaka hilo laini kuna mwamba katika hali ya geli yaani ni kati ya hali imara na hali kiowevu. Kwa hiyo vipande vyake havikai mahali pamoja lakini vina mikondo ndani yake kufuatana na mikondo ya joto kali inayopanda juu kutoka kiini cha dunia ambacho ni chuma cha moto katika hali kiowevu.
Mikondo hii inasukuma tabakamwamba ya nje na kuivunjavunja katika vipande au mabamba mbalimbali.
Kufuatana na nadharia ya gandunia, ganda la nje limevunjika na vipande vya ganda vyaitwa mabamba. Mabamba hayo yakaa juu ya koti moto kama majani yanayofunika maji katika sufuria inayopashwa moto. Maji ya moto huzunguka ndani ya sufuria na kusababisha majani usoni kutembea. Hivyo mabamba ya gandunia yana mwendo wakati wote.
Mwendo huo husababishwa na kupaa juu kwa magma (yaani mwamba moto wa kiowevu) inayotoka nje kwenye migongo iliyoko katikati ya sakafu ya bahari. Migongo hii ni safu ya milima ya kivolkeno chini ya maji, kwa mfano mgongo kati wa Atlantiki.
Magma hii inapoa kuwa mwamba mpya na kusukuma nusu mbili za bamba la kibahari kwenda nje. Pale ambapo bamba la kibahari linakutana na bamba la kibara linajisukuma chini yake kwa sababu miamba ya mabara ni myepesi na miamba ya bamba la kibahari ni zito zaidi. Hivyo pembizo la bamba la kibahari linazama chini na kuyeyuka katika joto la koti ya dunia. Eneo la kuzama chini linanonekana mara nyingi kama mfereji chini ya bahari.
Shindikizo hilo la sakafu ya bahari linasababisha pia mwendo wa bamba la kibara pamoja na kuvunjika kwa mabamba ya kibara.
Miendo ya gandunia imeunda uso wa dunia jinsi ulivyo na jinsi unavyoendelea kutokea na kubadilika.
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Gandunia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Gandunia, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.