Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu (pia: Tangazo la kilimwengu la haki za binadamu au Taarifa ya Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu, kwa Kiingereza: Universal Declaration of Human Rights) ni tamko la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu lililotolewa tarehe 10 Desemba 1948.
Ilikuwa kati ya maazimio ya kwanza kabisa ya UM.
Msingi wa haki hizo uko katika kifungo cha kwanza kinachosema, "Watu wote wamezaliwa huru, wakiwa na hadhi na haki sawa. Wamejaliwa akili na dhamiri na kupaswa kutendeana kwa roho ya kidugu".
Haki zinaorodheshwa katika vifungu 30 vinavyoeleza haki za msingi ambazo kila mtu anastahili kuwa nazo "bila kubaguana kwa rangi, taifa, jinsia, dini, siasa, fikra, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yoyote".
Haki zilizomo katika tangazo hili jinsi zilivyo si sheria ya kimataifa moja kwa moja, lakini zimekubaliwa na kila taifa lililojiunga na UM. Sehemu kubwa ya vipengele vyake imeingia katika mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiraia na kisiasa ya mwaka 1966 na mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya mwaka 1976 na kwa njia hiyo zimekuwa sehemu ya sheria za kimataifa.
Mawazo ya msingi ya tangazo la haki za binadamu ni pamoja na:
Azimio la UM si la kwanza katika historia kuorodhesha haki za binadamu. Mfano unaojulikana sana ni Tangazo la Haki za Kibinadamu na Kiraia lililotolewa na bunge la Ufaransa tarehe 26 Agosti 1789 wakati wa Mapinduzi ya Kifaransa.
Tamko la bunge la Ufaransa lilifuata katiba ya Marekani (4 Julai 1776) iliyotaja pia haki za msingi. Matangazo hayo yote mawili yanasimama kwenye msingi wa juhudi za falsafa ya zama za mwangaza katika karne ya 18, lakini mizizi yake katika ustaarabu wa Ulaya unategemea hadhi ya mtu kama sura na mfano wa Mungu katika imani ya dini ya Uyahudi na Ukristo.
Kwa kuwa kukiri heshima ya asili na haki sawa kwa binadamu wote ndio msingi wa uhuru, haki na amani duniani,
Kwa kuwa kutojali na kudharau haki za binadamu kumeletea vitendo vya kishenzi ambavyo vimeharibu dhamiri ya binadamu na kwa sababu taarifa ya ulimwengu ambayo itawafanya binadamu wafurahie uhuru wao wa kusema, kusadiki na wa kutoogopa cho chote imekwisha kutangazwa kwamba ndio hamu kuu ya watu wote,
Kwa kuwa ni lazima, ili mtu asishurutizwe kuomba msaada kutokana na maasi ya kupinga dhuluma na uonevu, kwamba haki za binadamu ziwe chini ya ulinzi wa sheria,
Kwa kuwa ni lazima kabisa kuendeleza uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa,
Kwa kuwa watu wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha tena katika Mkataba wao imani yao katika haki za asili, heshima na thamani ya binadamu na katika usawa wa haki kwa wanaume na wanawake, na kwa sababu wamekata shauri la kuendeleza mambo ya starehe na hali bora za maisha ya watu kwa kuwa na uhuru zaidi,
Kwa kuwa Nchi zilizo Wanachama zimeahidi, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kukuza na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wake wa asili,
Kwa kuwa kuzitambua haki hizi na uhuru huu ni jambo la maana sana kua kutimiza ahadi hiyo,
Kwa hiyo basi,
Baraza kuu linatangaza
Taarifa hii ya ulimwengu juu ya haki za binadamu kama ndio nguzo ya juhudi kwa watu wa mataifa yote ambayo hatimaye kila mtu na kila jamii ya watu - kwa kushikilia daima Taarifa hiyo - watajitahidi kufundisha jinsi ya kukuza heshima ya haki hizo na uhuru huo. Na mataifa yote yatajitahidi kuzifanya haki hizo zifahamike miongoni mwa Nchi zilizo Wanachama na miongoni mwa watu zinaowatawala.
Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu.
Kila mtu anastahili kuwa na haki zote za uhuru wote ambao umeelezwa katika taarifa hii bila ubaguzi wowote. Yaani bila kubaguana kwa rangi, taifa, wanaume na wanawake, dini, siasa, fikara, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yoyote. Juu ya hayo usifanywe ubaguzi kwa kutegemea siasa, utawala au kwa kutegemea uhusiano wa nchi fulani na mataifa mengine au nchi ya asili ya mtu, haidhuru nchi hiyo iwe inayojitawala, ya udhamini, isiyojitawala au inayotawaliwa na nchi nyingine kwa hali na namna yoyote.
Kila mtu ana haki ya kuishi, haki ya uhuru na haki ya kulinda nafsi yake.
Mtu yeyote asifanywe mtumwa au mtwana; utumwa na biashara yake ni marufuku kwa kila hali.
Mtu yeyote asiteswe, asiadhibiwe, asidharauliwe au kutendewa kinyama au kikatili.
Mbele ya sheria kila mtu ana haki ya kutambulika kama mtu.
Mbele ya sheria watu wote ni sawa na wanastahili haki sawa za kulindwa. Wote wana haki sawa ya kulindwa kutokana na ubaguzi wowote unaoweza kuvunja taarifa hii na mambo yoyote yanayoweza kuleta ubaguzi huo.
Kila mtu ana haki ya kutetewa na baraza la hukumu kwa makosa ya kuvunjiwa haki zake za asili anazostahili kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Mtu yeyote asikamatwe, asifungiwe au kuhamishwa kutoka nchi yake bila sheria.
Kila mtu ana haki kamili ya kuhukumiwa vyema hadharani na baraza lililo huru na lisilo na upendeleo katika kutoa uamuzi wa haki zake na wajibu wake na wa makosa yoyote yanayo-mhusu.
Kila mtu asiingiliwe bila sheria katika mambo yake ya faragha, ya jamaa yake, ya nyumbani mwake au ya barua zake. Wala asivunjiwe heshima na sifa yake. Kila mmoja ana haki ya kulindaw na sheria kutokana na pingamizi au mambo kama hayo.
Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo, dhamira na dini; haki hii inahusu pia uhuru wa kubadili dini yake au imani, na uhuru wa kubainisha hadharani au faraghani -akiwa peke yake au na watu wengine- dini yake kwa kufundisha kwa vitendo, kuabudu na kwa kuadhimisha.
Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na moni kwa njiayoyote bila kujali mipaka.
Kila mtu, kama raia, anayo haki ya kutunzwa na anastahili kupata haki zinazotokana na uchumi, starehe na utamadun-ambazo ni lazima kwa hali bora na maendeleo ya nafsi yake-kwa njia ya juhudi ya taifa na ushirikiano kati ya mataifa na kwa mujibu wa utaratibu na utajiri wa kila nchi.
Kila mtu ana haki ya kupumzika na kufanya kazi kwa kiasi cha saa zinazostahili.Pia ana haki ya kupata likizo, kwa kipindi na kupokea mshahara kama vile angekuwa kazini.
Ni haki kila mtu alindwe na taratibu au kanuni za jamii na zinazohusu mataifa mbalimbali ambazo ndani yake uhuru na haki zilizoelezwa katika taarifa hii zinzweza kuhifadhiwa barabara.
Hakuna maneno yoyote katika taarifa hii yanayoweza kubashiriwa kwamba yanaruhusu nchi yoyote, kikundi cha watu au mtu fulani kufanya au kushughulika na jambo lolote ambalo nia yake ni kuharibu haki na uhuru zilizoelezwa humu.
Makala hii kuhusu mambo ya sheria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu kama historia yake au uhusiano wake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
This article uses material from the Wikipedia Kiswahili article Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu, which is released under the Creative Commons Attribution-ShareAlike 3.0 license ("CC BY-SA 3.0"); additional terms may apply (view authors). Maudhui yanapatikana kwa chini ya CC BY-SA 4.0 isipokuwa iwe imebainishwa vinginevyo. Images, videos and audio are available under their respective licenses.
®Wikipedia is a registered trademark of the Wiki Foundation, Inc. Wiki Kiswahili (DUHOCTRUNGQUOC.VN) is an independent company and has no affiliation with Wiki Foundation.